Katika Ulimwengu wa sasa na hasa Tanzania yetu bado kuna vijana wengi wanaoamini kuwa na mafanikio ya kibiashara unahitaji mtaji mkubwa. Lakini wapo wajasiriamali wakubwa ambao wamefanya vizuri kutokana na ubunifu wao katika kukuza biashara.
Gazeti na Mtandao wake maarufu zaidi duniani la Forbes unamtaja mtanzania Said Salim Bakhresa kuwa amefanya mauzo yanayofikia dola milioni 800 za Marekani katika mwaka huu wa 2016-Ingawa bado haujaisha, Hivyo kuwa katika nafasi ya tatu kati ya wajasiriamali wenye pato la juu zaidi(Matajiri) nchini Tanzania akiwafuatia Mohammed Dewji na Rostam Azizi
Bakhresa ni nani?
Said Salim Bakhresa alizaliwa mwaka 1949 mjini Zanzibar, alisoma elimu ya msingi hadi alipofikia umri wa miaka 14 ambapo aliacha shule kutokana na maisha ya familia kuwa magumu hivyo kujiingiza katika biashara ili aweze kuhudumia familia katika mahitaji kama chakula baada ya baba yake kukabiliwa na madeni. Ingawa haipo wazi alianza na mtaji wa kiasi gani, Lakini alikuwa maarufu kwa biashara ya viazi vya kuchemsha.
Miaka ya 1960, Bakhresa alijiingiza katika biashara ya kununua mabaki ya mazao ya baharini kama, mifupa na magamba ya viumbe wa baharini na kuyauza Mombasa. Kutokana na tofauti ya kifedha iliyokuwapo wakati huo(Kati ya Tanzania na Kenya), aliweza kununua ngozi za viatu kutoka Kenya na kuzitumia kushonea viatu hapa Tanzania.
Katika miaka ya 1970 aliamua kuirudia biashara yake ya viazi lakini wakati huu aliongeza mikate na kisha kuununua mgahawa toka kwa mgeni wa kihindi ukiwa na jina la AZAM,jina ambalo analitumia kama nembo(brand) ya bidhaa zake kwa sasa. Aliuendesha na kuusimamia mgahawa huu kwa mafanikio makubwa.
Hatimaye miaka ya 1990 alianza uwekezaji katika biashara za nafaka hasa Ngano na Mchele. Biashara ilikuwa na kugeuka kuwa viwanda vikubwa kabisa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati. Kwa sasa kiasi kikubwa cha mchele na bidhaa za nafaka zinatoka katika kampuni ya Bakhresa Group iliyopo Kipawa (Flour Mill). Mfano tu nchini Zimbabwe, amewekeza mwaka huu takribani dola milioni 30 za Marekani ili kumiliki kiwanda kikubwa cha nafaka cha Blue Ribbon(BRI). Nchi jirani ya Rwanda, inategemea tani 120,000 za unga wa Ngano kwa mwaka kutoka kwa kampuni za Bakhresa.
Miaka ya 2000 imekuwa ni ya mafanikio zaidi kwake, nembo yake ya Azam imekuwa maarufu zaidi katika soko la Ndani na Nje, hata sasa kuna msemo ‘’ Ukiamka Azam, Ukitembea Azam, Ukilala ni Azam’’ yaani bidhaa za kampuni yake zimetawala katika maisha ya kawaida.
‘’Asubuhi tuamkapo tunapata kifungua kinywa kwa vitafunwa vya Azam. Mchana tunakula ugali, wali, au chips na tunakunywa maji na juice kutoka Azam. Jioni kama utakula tambi au kunywa soda n.k’’ Pia mtu anayekuwa na fedha kidogo pia huitwa Bakhresa.
Kulingana na jarida la Forbes Bakhresa ndiye akishikilia nafasi ya 30 ya matajiri Afrika. Huku akitoa ajira kwa watu zaidi ya 5,000 wenye ajira rasmi.
Mjasiliamali huyu amejijengea umaarufu mkubwa katika biashara kwa takribani miongo mitatu sasa. Ameweza kujenga timu imara ambayo inasimamiwa na wakurugenzi makini ambao ni watoto wake mwenyewe. Bakhresa Group ina matawi katika nchi sita ambazo ni,. Rwanda, Burundi, Uganda, Malawi, Zambia na Msumbiji. Amejikita zaidi katika usindikaji wa vyakula. Ana viwanda vya kusaga unga wa ngano na mahindi, viwanda vya ukoboaji wa mchele, uandaaji wa vyakula kama mikate,chapatti, vinywaji kama maji (Uhai) , juisi za matunda na soda, pamoja na ice cream. Pia ana kiwanda cha vifungashio vya bidhaa mbalimbali, biashara ya mafuta ya magari na mitambo. Vilevile anazo boti za usafilishaji abiria ambazo hufanya safari zake katika Bahari ya Hindi. Hali kadhalika, anafanya biashara ya usafirishaji mizigo (Azam logistics). Katika michezo ,Bakhresa anamiliki timu ya mpira wa miguu ijulikanayo kwa jina la Azam Footbal Club ambayo imefikia kiwango cha kucheza ligi kuu Tanzania bara na mabingwa wa soka Tanzania Bara msimu 2013/2014.
Said Salim Bakhresa unamzungumzia mtu wa aina yake katika Tanzania, ni mtu anayesemekana kusimamia maono yake na kuhakikisha yanatimilika kikamilifu. Anauzoefu mkubwa katika usimamizi wa biashara , ni mtu anaye fanya tafiti juu ya maendeleo ya viwanda na masoko katika kutambua mahitaji ya watu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Anatumia mbinu mbalimbali katika kuhakikisha bidhaa zake zinaliteka soko la ndani na la nje ya nchi. Licha ya kutangaza bidhaa zake kupitia redio na televisheni, anapata fursa ya kujitangaza kupitia timu yake ya mpira wa miguu anayoimiliki(Azam Football Club) hivyo anatangaza bidhaa zake kupitia michezo. Vilevile anawatumia wachuuzi au Machinga katika kutangaza bidhaa zake mfano Ice cream. Pamoja na mafanikio makubwa aliyonayo , mfano kumiliki na kuendesha biashara mbalimbali ndani na nje ya nchi , bado kuna vikwazo na changamoto mbalimbali anazokabiliana nazo ili kufikia malengo yake.
Katika suala zima la kupanga , kudhubutu na kufanya ni vitu vya msingi katika kufikia mafanikio. B akhresa ni mtu anayehamasisha Watanzania wasiogope kujifunza kwa vitendo, kwani wengi huhofia changamoto zinazoweza kusababisha, anguko katika biashara lakini mjasiliamali anapaswa kujiamini katika mawazo yake na kujiwekea mipango mathubuti. Ka zi ya ujasiliamali inahitaji ubunifu kwa kiasi kikubwa katika kuweza kubaini na kuibua fursa zilizopo na hata kuweza kukabiliana na changamoto zake.
Kwa sasa bado Bakhresa anaendelea kutanua wigo wa biashara katika kuweza kufikia nchi nyingi zaidi duniani. Hata hivyo anaamini kwamba bidhaa zake bado hazijatosheleza soko la ndani . Bado anazitizama fursa zilizopo katika soko la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Hivyo basi anajitahidi katika kuboresha bidhaa zake zaidi ili kuhakikisha zinakuwa na ubora unaotakiwa na hatimaye kushikilia soko la kitaifa na kimataifa.
Mwishoni, Mafanikio ya Bakhresa ni mengi sana, Ila anatufunza vijana kuwa wabunifu, wenye jitihada na nidhamu ya kutosha katika kila tunachokifanya. Siamini kama Bakhresa angetumia muda wake mwingi kufuatilia ‘series’ za Marekani au kufanya yasiyofaa angefika hapo. Amka kijana usiishi kwa ndoto.
0 Comments