MAKOSA 14 HATARI YANAYOFANYWA NA WASANII WENGI TANZANIA


MAKOSA 14 HATARI YANAYOFANYWA NA WASANII WENGI TANZANIA


Kama unataka kupata michongo zaidi, kuwavutia watu waje kwenye show yako au kuuza nyimbo zako, hakuna dawa yoyote unayoweza kuweka kwenye
nyimbo zako. Ingawa kutoa nyimbo nzuri kunasaidia lakini unatakiwa kuwa na mtazamo na muonekano utakaovutia watu kwa kile unachofanya na pia kuelewa jinsi mchezo wa biashara ya muziki unavyochezwa
Haya ni baadhi ya makosa 14 ya mara kwa mara ambayo wasanii wengi hufanya.
 1.Kuishi nyumaya muda katika ulimwengu ambao haukuwa na mitandao ya kijamii

Ujio wa mitandao ya kijamii kama Facebook na Twitter umerahisisha mawasiliano kwa kiasi kikubwa. Imerahisisha mawasiliano kati ya wasanii na mashabiki wao au wasanii na vyombo vya habari.

Sentensi fupi kama ‘September 29 ni siku yangu muhimu, ntazindua album yangu mpya, naombeni support yenu’ kwenye Facebook au Twitter inaweza kusafiri mamilioni ya maili na kuwafikia mashabiki wako wengi duniani kote na vyombo vya habari vikapata habari. Bahati mbaya ni kwamba kuna wasanii wengi wenye allergy na mitandao ya kijamii.

Haijulikani wako wapi, wanafanya nini, wanatoa lini wimbo mpya na kwa ufupi ni kwamba wamejichimbia shimoni. Kama haupo Facebook, Instagram wala Twitter, unategemea jina lako liongelewe wapi?

2.Kuanika kila kitu kwenye mitandao ya kijamii

Hakuna haja ya kuandika kwenye Twitter au Facebook kuhusu promoter wa Kahama aliyeshindwa kukulipa hela yako ya show na ukakosa nauli ya kurudi Dar es Salaam. Haikusaidii chochote zaidi ya kukushusha. Blogs zitasherehekea kwakuwa zitakuwa zimepata habari nzuri ya kuvuta traffic na kukuchoresha zaidi wewe kwa vichwa vya habari kama ‘Ugolo Mweupe akosa nauli ya kurudi Dar baada ya promoter kumwacha kwenye mataa’.

Wewe ni staa. Unaishi ndoto. Itunze ndoto hiyo. Usimwambie kila mtu jinsi ulivyopigika na kwamba bado unaishi na mama yako ama kitu chochote kinachoweza kuharibu heshima kwa mashabiki wako. Kumbuka hauuzi tu muziki wako bali pia unauza wajihi wako.

3. Kupenda kuponda wasanii wenzako, vyombo vya habari ama wadau wengine hadharani

Kuna wasanii wanaojiona wao ndio kila kitu. Wao ndio rappers ama waimbaji bora tangu ulimwengu uanze. Mara nyingi tumesikia wasanii wakihojiwa redioni na kuanza kuponda nyimbo za watu wengine kana kwamba nyimbo zao zimetungwa kwa msaada wa malaika. Japokuwa una haki ya kutoa maoni yako pia unapaswa kukumbuka kuwa suala la kukosoa nyimbo hadharani ni kazi ya wachambuzi wasiofungamana na upande wowote. Unapokosa wimbo wa mwenzio na kumuita wack mcee, tambua kuwa kuna mashabiki wengi wanaoumpenda na kwa namna yoyote utakuwa umewakera pia.

Nakumbuka niliwahi kusikia interview ya Hammer Q kwenye kipindi cha Leo Tena Clouds FM na kumsikia jinsi alivyokuwa akiwadhalilisha madj wa redio zingine kuwa wanaendekeza rushwa. Japokuwa suala hilo kweli lipo, lakini hakupaswa kuzungumza hivyo kwenye radio inayosikilizwa nchi nzima. Nina uhakika siku hiyo alizungumza ujumbe uliowakera watu wa radio zingine nyingi ambao kuanzia siku hiyo walimuona snitch.

4. Kutokuwa rafiki wa vyombo vya habari

Ni ngumu kuwa karibu na redio, TV, magazeti ama blogs zote nchini lakini ni muhimu kuziheshimu zote. Ukiombwa interview na kituo cha radio cha Ludewa, unapaswa kuwa na muitikio sawa na kama unapoombwa interview na radio kubwa ya Dar es Salaam. Unapokuwa msanii mkubwa, tambua kuwa kila kona ya nchi kuna mashabiki wako, hivyo usiwanyime fursa mashabiki wako wa vijijini kujua habari zako.

5. Kuachia nyimbo kwa mfumo wa Exclusive

Niliwahi kuandika mada hii kwa urefu zaidi hapa. Lakini ninao mfano halisi wa msanii mkubwa aliyeniambia kuwa kipo kituo kikubwa kimoja cha redio ambacho hakipigi tena nyimbo zake kwasababu alichagua kwenda kuutambulisha wimbo wake exclusive kwenye kituo kingine cha redio.

6. Kuwa mikononi mwa meneja asiyekijua kiwanda cha muziki

Asilima kubwa ya wasanii, hasa wachanga wapo chini ya mameneja wenye pesa lakini wasio na ufahamu wa namna muziki wa Tanzania ulivyo. Wengi humsaidia msanii kwa kipindi fulani akitegemea matunda yaanze kuonekana ndani ya miezi mitatu.

Kwa mazingira ya muziki ulivyo Tanzania ni ndoto kupata mafanikio katika kipindi hicho. Ni bora kuwa na meneja mwenye kipato cha kawaida lakini anayezijua njia na fitina za muziki wa Tanzania, kuliko kuwa na meneja mwenye hela lakini anayeishi kwenye ulimwengu tofauti na ule wa muziki.

7. Kufulululiza kutoa nyimbo zinazofanana

Kuna kichaa mmoja alipita sehemu na kuokota noti ya shilingi elfu moja. Basi kuanzia siku hiyo, alihakikisha anapita eneo hilo zaidi ya mara 20 akitegemea kuwa ataokota tena hela nyingine. Huo ni mfano wa namna baadhi ya wasanii wa Tanzania walivyo. Wimbo mmoja ukiwa hit, basi atahakikisha zingine mbili mpya zitakuwa ama na beat inayofanana na ya mwanzo ama ujumbe/mashairi sawa na wa mwanzo. Kwa mfumo huo, ni ndoto kufululiza kutoa hits bali utakuwa kama unaachia series au remix za nyimbo zako.

8. Kutokuwa na producer mmoja anayekupatia

Simaanishi kuwa kila msanii awe na producer mmoja tu wa nyimbo zake. Maana yangu ni kwamba, kuna namna ambavyo inatokea producer mmoja humpatia zaidi msanii fulani.

Kwa Tanzania tunafahamu jinsi Mika Mwamba anavyompatia Mad Ice, Mona G anavyowapatia Young Killa na Belle 9, marehemu Roy alivyokuwa akiwapatia Mr Blue na Abby Skillz, KGT anavyompatia Ali Kiba, John Mahundi anavyompatia Crazy GK, P-Funk alivyompatia Jay Mo, Juma Nature na wengine.

Mfano wa Marekani, Timbaland anavyompatia Justin Timberlake, 40, Matthew Jehu Samuels Boi-1da na T-Minus wanavyompatia Drake, vocals zote za nyimbo za Rihanna hufanyiwa kazi (produced) na Makeba Riddick aka Girl Wonder, nyimbo karibu zote za Jay-Z lazima zipitie mikono ya Rick Rubin na wengine.

9. Kutafuta Kiki

Kila mmoja anapenda kupata Kiki lakini wakati mwingine Kiki zimewatokea puani wasanii wengi. Tafuta kile ninachoweza kukiita ‘Intelligent Kick’ na sio ‘Mediocre Kick’.

10. Timing ya kuachia wimbo

Unapofikiria muda wa kuachia wimbo inabidi utulize akili kidogo sababu unaweza kujikuta ukitupa jiwe gizani. Angalia muda mzuri wa kuachia wimbo usije ukaachia katika muda ambao wimbo wake utapotea kwenye rotation baada ya wiki moja tu.

11.Kutojipigia debe

Hivi karibuni nilipiga story na rapper Wakazi na akanieleza jinsi anavyofanya mambo yake. Kwa kiasi kikubwa jina lake limefahamika kwa jitihada zake mwenyewe na tena kwa promotion ya online. Alikuwa akihangaika mwenyewe kujipigia promo kupitia mitandao ya kijamii na kushirikisha blog zingine. Baada ya kuona watu wengine wa blog wanambania, akafungua blog yake mwenyewe kibishi na kuandika issue zake. Ukiwa mmoja wa followers wake, unaweza kugundua kirahisi jinsi anavyojipromote mwenyewe kwa kuandika tweets kama; Pls Request “Touch” by Wakazi on your favorite radio station.
Usipojipromote mwenyewe, ni nani mwingine atafanya hivyo?

12. Kulazimisha kushawishi watu wasikie/wacheze wimbo wako

Haina haja ya kulazimisha watu kwa kuwatag Facebook wasikilize nyimbo zako online. Mara nyingi ukiwa msanii msumbufu wa kuwapigia simu watangazaji kila siku na meseji zisizo na kichwa wala miguu, unajiweka cheap na kujishusha.

Kama mtangazaji hajaupenda wimbo wako kwakuwa ni kweli si mzuri, usijaribu kumshawishi kwasababu, kama ni mbovu hatoucheza. Na kadri unavyoendelea kumsumbua acheze wimbo wako, ndivyo anavyokumbuka jinsi ulivyogeuka kero kwake.

Hiyo ina maana kuwa utajiharibia hata kwenye ngoma zako zijazo.

13. Kushindwa kutengeneza uhusiano mzuri na mashabiki wako

Hakuna mtaji mkubwa kama mashabiki. Kama utakuwa na uhusiano nao mzuri, hawatakuangusha kamwe. Watu si wajinga. Wanafahamu sana pindi unapotaka wanunue ama wasikilize kazi zako. Kama una uhusiano mzuri na mashabiki wako na wanajua unawajali watakusupport kwa kila kitu.

Kwenye makala yake aliyoipa jina; ‘6 lessons artists must learn from ‘anacondagate’ Mwandishi na gwiji wa masuala ya Masoko, Constantine Magavilla aliandika:

Loyal fans outstrip money in the long run so never undermine them. They will come out and support you when you need them most! The worst thing you can do is not to appreciate your fans when you are on top of the world. Remember, your social significance and earnings are a function of the number fans you have and the value each brings to the table.”
Kila siku – haijalishi upo busy ukirekodi, kwenye tour, au ukiwa nyumbani na wasiwasi jinsi gani utapata fedha za kufanya video mpya – fanya kitu (haijalishi kiwe kidogo vipi) kuwafikia mashabiki wako.

14. Kutoa video iliyo chini ya kiwango cha ukubwa wa wimbo

Video inafahamika kwa jinsi inavyoupa uhai wimbo. Kama ukifanya video nzuri ya hit yako, basi ukubwa wa wimbo utaongezeka mara dufu. Lakini kama ukifanya video ya kawaida ama iliyo chini ya kiwango cha ukubwa wa wimbo, video hiyo itaichimbia kaburi refu ngoma hiyo.
Imeandaliwa na @star_king_worldwide
                www.wasaport.blogspot.com

Post a Comment

0 Comments